Friday, April 25, 2014

MAKALA MAALUM

MUUNGANO WETU

African Brotherhood Foundation (ABF) ni  taasisi changa yenye malengo na  nia thabiti ya kuwaunganisha waafrika wote katika nyanja zote za kijamii, kiuchumi na kisiasa. Tunaamini kiu kubwa ya waafrika ni kuona Afrika inaungana na sio kutengana, sisi tumeamua kulisimamia suala hili ili kutimiza ndoto za waasisi  na wapambanaji wa harakati za umoja wa Afrika . Leo hii katika bara la Afrika muungano tuliokuwa  nao wa pekee ni wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania.

Kama ilivyokua ada kila mwaka ifikapo tarehe 26 mwezi wa 4 watanzania tunakumbuka na kuadhimisha kuzaliwa kwa nchi yetu ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania. Nchi hii imetokana na zilizokuwa nchi mbili za wakati huo Jamuhuri ya Tanganyika na Jamuhuri ya watu wa Zanzibar chini ya viongozi wakuu wa nchi hizo ambao ni hayati mwalimu Julius Kambarage Nyerere rais wa Tanganyika na Hayati shekhe Abeid Aman Karume rais wa Zanzibar waliweza kuafikiana na kuunganisha nchi hizo kwa maridhiano ya hali ya juu baada hapo ndipo Jamuhuri ya muungano wa Tanzania ikaanza kutambulika  katika medani za kimataifa. Hivi sasa ni miaka 50 toka kuzaliwa kwa muungano huo na kuipata nchi yenye sifa kubwa katika mataifa mbalimbali ndani ya bara la Afrika na kote ulimwenguni. Imefikia wakati raia wa  nchi hii wanajivunia utanzania wao kufatia matunda yatokanayo na muungano wetu huu wa kihistoria.

 Kuna baadhi ya nchi ndani ya Afrika zilijaribu kuungana lakini zikashindwa kuendesha muungano wao ndani ya  muda mfupi ukavunjika mfano Senegambia uliokuwa muungano kati ya nchi za Senegali na Gambia ambao historia inaonyesha nchi hizi mbili mila zao na tamaduni zinafanana lakini walishindwa kuvumiliana na kuaminiana kwa pamoja ilikujenga muungano wao. Dhumuni ya kuendesha muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar ni kulinda utu wa muafrika, usalama, kukuza uchumi wa nchi hizi,  kuwezesha muingiliano wa watu wa pande zote mbili na kuifanya Afrika yetu iweze kuungana kwa pamoja ili kuepuka vita vya wenyewe kwa wenyewe.


 Tunaelewa kabisa katika muungano wetu huu kunachangamoto ambazo zinahitaji busara na hekima za watu wa nchi hii wakiwamo viongozi na raia wa kawaida kuweza kuzitatua bila ya hiyana yeyote ile. Kuna baadhi ya watu wanajaribu kuchomoza na hoja zao dhaifu na kutaka kuuvunja muungano kwa madai wamechoshwa na muungano ni bora uvunjike, sawa ni uhuru wakujielezea inaotokana na katiba ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 18 kifungu (A), lakini tusitumie uhuru huu kwa kuwapotosha watu wa nchi hii tukifanya hivyo basi tuwe tayari historia kutuhukumu sisi na vizazi vinavyokuja. Waliopigania muungano huu hawa kuwa wajinga hata kidogo walitanguliza maslahi ya nchi kwanza na Afrika ndio maana ukapatikana muungano huu tulionao hivi sasa, hivyo tunao wajibu wa kuulinda kwa gharama yeyote ile ili muungano wetu usivunjike. 


Leo hii tunajua kabisa mwananchi wa Micheweni, Machomane, Jang’ombe hata Kilimani hawana matatizo na wananchi wa Ifakara,  Msoga, Bariadi , isipokua kuna baadhi ya watu walio wabinafsi wanataka tofauti na mitafaruku itokee sisi ni mashahidi wa yale yanayo tokea sudani ya kusini wala haya hitaji mwalimu atufundishe bali akili zetu zinafanya kazi katika kutafakuli na kuyachambua yanayo wasibu ndugu zetu wale,hivyo basi tutumie mfano ule kama funzo tosha kwetu katika kuakikisha tunalinda muungano wetu. Tukumbuke tunajivunia utanzania tuliokuwa nao kutokana na muungano wetu ,amani hii tunaoiona ni mbegu zilizopandwa 26/4/1964 na sasa tunavuna matunda ya utulivu hivyo kila mmoja wetu anao wajibu wa kuulinda muungano huu tuache porojo ambazo zitatupelekea kwenye dimbwi la machafuko wengine mkakimbilia ughaibuni mkaacha raia wanapata shida zitakazo ipoteza nchi yetu kwenye ramani ya amani na utulivu.


Sisi African Brotherhood Foundation(ABF) wito wetu kwa serikali ya Jamuhuri ya muungIano wa Tanzania waache kulewa na madaraka badala yake wasikilize kero za wananchi  na wawe tayari kuzishughulikia ili ufumbuzi  uweze kupatiana kwa urahisi. Jukumu lao kuu ni kuulinda muungano pia wanawajibu wa kulinda rasilimali zetu na kuondoa umasikini,ujinga,na maradhi itasaidia kupunguza kero za muungano kwa asilimia kubwa na kuwafanya watu kuwa wamoja na hata wale wasio utakia mema watashindwa pakuanzia. Hapa uzalendo unatakiwa ili kuupata muundo utakao leta tumaini katika muungano wetu, vilevile mnatakiwa kufanya mambo yenu kwa uwazi ili kupunguza tuhuma na malalamiko ya kila wakati kwa serikali hususani katika suala hili nyeti la muungano tujitahidi kuiga mema yaliofanywa na waasisi wa taifa hili kwani walikuwa waumini wa muungano na wapingaji wa sera za unyonyaji ndio maana walifanya jitihada kupatikana kwa muungano huu.


 Mwisho wale wanaodhani wanaweza kututenganisha wakumbuke sisi ni waumini wa muungano hivyo basi hawana nafasi yeyote ya ushawishi kwetu,kama wanaweza basi wautenganishe ule mchanga uliochanganywa  na mzee Nyerere pamoja na mzee Karume. Tusisubiri maadhimisho ya kila mwaka bali tunawajibu wa kukumbuka muungano na kuulinda siku zote za maisha yetu Afrika kwanza mimi baadae.

 
ONE BLOOD, ONE LOVE, ONE AFRICA FOREVER!