Friday, April 25, 2014

MAKALA MAALUM

MUUNGANO WETU

African Brotherhood Foundation (ABF) ni  taasisi changa yenye malengo na  nia thabiti ya kuwaunganisha waafrika wote katika nyanja zote za kijamii, kiuchumi na kisiasa. Tunaamini kiu kubwa ya waafrika ni kuona Afrika inaungana na sio kutengana, sisi tumeamua kulisimamia suala hili ili kutimiza ndoto za waasisi  na wapambanaji wa harakati za umoja wa Afrika . Leo hii katika bara la Afrika muungano tuliokuwa  nao wa pekee ni wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania.

Kama ilivyokua ada kila mwaka ifikapo tarehe 26 mwezi wa 4 watanzania tunakumbuka na kuadhimisha kuzaliwa kwa nchi yetu ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania. Nchi hii imetokana na zilizokuwa nchi mbili za wakati huo Jamuhuri ya Tanganyika na Jamuhuri ya watu wa Zanzibar chini ya viongozi wakuu wa nchi hizo ambao ni hayati mwalimu Julius Kambarage Nyerere rais wa Tanganyika na Hayati shekhe Abeid Aman Karume rais wa Zanzibar waliweza kuafikiana na kuunganisha nchi hizo kwa maridhiano ya hali ya juu baada hapo ndipo Jamuhuri ya muungano wa Tanzania ikaanza kutambulika  katika medani za kimataifa. Hivi sasa ni miaka 50 toka kuzaliwa kwa muungano huo na kuipata nchi yenye sifa kubwa katika mataifa mbalimbali ndani ya bara la Afrika na kote ulimwenguni. Imefikia wakati raia wa  nchi hii wanajivunia utanzania wao kufatia matunda yatokanayo na muungano wetu huu wa kihistoria.

 Kuna baadhi ya nchi ndani ya Afrika zilijaribu kuungana lakini zikashindwa kuendesha muungano wao ndani ya  muda mfupi ukavunjika mfano Senegambia uliokuwa muungano kati ya nchi za Senegali na Gambia ambao historia inaonyesha nchi hizi mbili mila zao na tamaduni zinafanana lakini walishindwa kuvumiliana na kuaminiana kwa pamoja ilikujenga muungano wao. Dhumuni ya kuendesha muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar ni kulinda utu wa muafrika, usalama, kukuza uchumi wa nchi hizi,  kuwezesha muingiliano wa watu wa pande zote mbili na kuifanya Afrika yetu iweze kuungana kwa pamoja ili kuepuka vita vya wenyewe kwa wenyewe.


 Tunaelewa kabisa katika muungano wetu huu kunachangamoto ambazo zinahitaji busara na hekima za watu wa nchi hii wakiwamo viongozi na raia wa kawaida kuweza kuzitatua bila ya hiyana yeyote ile. Kuna baadhi ya watu wanajaribu kuchomoza na hoja zao dhaifu na kutaka kuuvunja muungano kwa madai wamechoshwa na muungano ni bora uvunjike, sawa ni uhuru wakujielezea inaotokana na katiba ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 18 kifungu (A), lakini tusitumie uhuru huu kwa kuwapotosha watu wa nchi hii tukifanya hivyo basi tuwe tayari historia kutuhukumu sisi na vizazi vinavyokuja. Waliopigania muungano huu hawa kuwa wajinga hata kidogo walitanguliza maslahi ya nchi kwanza na Afrika ndio maana ukapatikana muungano huu tulionao hivi sasa, hivyo tunao wajibu wa kuulinda kwa gharama yeyote ile ili muungano wetu usivunjike. 


Leo hii tunajua kabisa mwananchi wa Micheweni, Machomane, Jang’ombe hata Kilimani hawana matatizo na wananchi wa Ifakara,  Msoga, Bariadi , isipokua kuna baadhi ya watu walio wabinafsi wanataka tofauti na mitafaruku itokee sisi ni mashahidi wa yale yanayo tokea sudani ya kusini wala haya hitaji mwalimu atufundishe bali akili zetu zinafanya kazi katika kutafakuli na kuyachambua yanayo wasibu ndugu zetu wale,hivyo basi tutumie mfano ule kama funzo tosha kwetu katika kuakikisha tunalinda muungano wetu. Tukumbuke tunajivunia utanzania tuliokuwa nao kutokana na muungano wetu ,amani hii tunaoiona ni mbegu zilizopandwa 26/4/1964 na sasa tunavuna matunda ya utulivu hivyo kila mmoja wetu anao wajibu wa kuulinda muungano huu tuache porojo ambazo zitatupelekea kwenye dimbwi la machafuko wengine mkakimbilia ughaibuni mkaacha raia wanapata shida zitakazo ipoteza nchi yetu kwenye ramani ya amani na utulivu.


Sisi African Brotherhood Foundation(ABF) wito wetu kwa serikali ya Jamuhuri ya muungIano wa Tanzania waache kulewa na madaraka badala yake wasikilize kero za wananchi  na wawe tayari kuzishughulikia ili ufumbuzi  uweze kupatiana kwa urahisi. Jukumu lao kuu ni kuulinda muungano pia wanawajibu wa kulinda rasilimali zetu na kuondoa umasikini,ujinga,na maradhi itasaidia kupunguza kero za muungano kwa asilimia kubwa na kuwafanya watu kuwa wamoja na hata wale wasio utakia mema watashindwa pakuanzia. Hapa uzalendo unatakiwa ili kuupata muundo utakao leta tumaini katika muungano wetu, vilevile mnatakiwa kufanya mambo yenu kwa uwazi ili kupunguza tuhuma na malalamiko ya kila wakati kwa serikali hususani katika suala hili nyeti la muungano tujitahidi kuiga mema yaliofanywa na waasisi wa taifa hili kwani walikuwa waumini wa muungano na wapingaji wa sera za unyonyaji ndio maana walifanya jitihada kupatikana kwa muungano huu.


 Mwisho wale wanaodhani wanaweza kututenganisha wakumbuke sisi ni waumini wa muungano hivyo basi hawana nafasi yeyote ya ushawishi kwetu,kama wanaweza basi wautenganishe ule mchanga uliochanganywa  na mzee Nyerere pamoja na mzee Karume. Tusisubiri maadhimisho ya kila mwaka bali tunawajibu wa kukumbuka muungano na kuulinda siku zote za maisha yetu Afrika kwanza mimi baadae.

 
ONE BLOOD, ONE LOVE, ONE AFRICA FOREVER!

Friday, March 7, 2014

MAKALA MAALUM

MWANAMKE NI MAMA WA DUNIA


African Brotherhood Foundation (ABF)  ni  taasisi changa yenye malengo na  nia thabiti ya kuwaunganisha waafrika wote katika nyanja zote za kijamii, kiuchumi na kisiasa. Hivyo basi tunaamini kiu kubwa ya waafrika ni kuona Afrika inaungana, sisi tumeamua kulisimamia suala hili ili kutimiza ndoto za waasisi wa umoja wa Afrika  ambao nyuma yao walikuwepo wanawake katika mapambano ya kutafuta uhuru wa bara la Afrika.
Mtazamo wa  African  Brotherhood  Foundation, kama ilivyo siku zote katika dunia, mungu ameumba vitu mbalimbali kwa maana yake. Leo hii kona ya ABF Africa imeona igusie na kuelezea  juu  ya mwanamke. Kimantiki  ndani ya dunia hakuna mwanadamu asiye zaliwa na mwanamke na watu wote ni lazima tuwathamini wanawake.  Sifa za mwanamke katu hatuwezi kuzimaliza kwa maana thamani yake ni kubwa na zenye kuvutia ukizisikiliza na kuziona. Katika bara letu la Afrika wanawake wana mchango mkubwa sana. Busara zao ndizo zilichangia Afrika kuwa huru mpaka hivi sasa ingawa  wadai uhuru wa  nchi nyingi za Afrika walikuwa ni wanaume. Lakini ukitazama utaona mwanamke alikuwa nyuma ya mwanaume kwa kumpa mawazo na muelekeo mzuri ndio maana mambo yalikwenda kwa kasi na uweledi kwasababu kama tunavyo jua mwanamke akilala jamii imelala.
Hebu tazama mwanamke alivyokuwa mbunifu. Familia nyingi za bara hili la afrika zinategemea uwepo wa mwanamke ili ziweze kupata maendeleo ya mali, chakula na hata mavazi. Hii ni kwa sababu yeye ndiye chanzo cha ufanisi katika jamii kwenye kutimiza wajibu wa kila siku. Mungu aliwaumba kwa makusudio maalumu ya kuisaidia na kuikomboa jamii sio kuwa wasindikizaji kama madai ya baadhi ya watu wenye fikra potofu na mawazo mgando. Kona ya ABF Africa inapenda kuwaambia watu wanaonyanyasa wanawake waache mara moja, hivi nyie hamna huruma wala chembe ya ubinadamu hata kidogo? Mama amebeba ujazito wako miezi tisa, amejifungua kwa uchungu na kukulea kwa shida na dhiki na kufikia kipindi chakula nyumbani hakuna aliweza kutumia maarifa ya ziada kwa kuchemsha mawe ili akupe moyo na kutuliza njaa yako? Vilevile kufanya jitihada kwa kupata chakula kwa siku inayo fuata iwe kwa kukopa au njia nyingine lakini leo hii wewe binadamu usiye na huruma wala shukurani kwa mwanamke unamdharau na kumnyanyasa! Tambua amani unayo iona hii imetokana na yeye kwa sababu ndiye chanzo cha amani duniani kwa ujumla kutokana analeta utulivu na kuzuia jazba za kina baba majumbani. Leo  sisi ni mashuhuda viongozi wengi wanapendeza na kupanda majukwaani na kujinasibu ni kazi kubwa  inayofanywa na wanawake kwa utashi mkubwa waliopewa na mungu.
 Asiye mpenda mwanamke asipewe kipaumbele cha aina yeyote ile katika jamii, ushujaa wa mwanamke upo kwenye mafungu yote ya kinadharia na kivitendo. Mtazamo wa kona ya ABF Afrika ni kuona Afrika inaungana ili kukata kiu kubwa ya watu wengi wa bara letu. Hii ndio maana imeamua kumuelezea mwanamke kwa kutambua kabisa bila ya yeye kuwepo na kushirikishwa muungano tunao upigania hauwezi kupatikana bila michango yao. Na kwa kulifahamu hilo ni lazima tuwashirikishe moja kwa moja na kuungana nao kwenye harakati zao zote za mabadiliko kimaneno na vitendo.
Jamii za kiafrika zinapaswa zibadilike ili ziweze kupata maendeleo vilevile zitambue kwenye kila jambo la kimaendeleo kuna mwanamke, kona ya ABF Afrika itaendelea kulaani mateso, ukandamizaji, ukatili na unyanyasaji dhidi ya mwanamke bila ya kificho wala uwoga wa aina yeyote. Kama taasisi changa ya AFRICAN BROTHERHOOD FOUNDATION (ABF) kwa pamoja tunatambua mchango mkubwa unaofanywa na mwanamke, huu sio wakati wa kulalamika, mtumie fursa za kujenga hoja zenye mantiki na zenye kuleta mabadiliko kwenye jamii za kiafrika. Kwa maana hiyo kushirikiana na mwanamke kutaleta misingi ya uzalendo, utawala bora, umoja na mshikamano wa hali ya juu kwa bara la Afrika.
Vilevile tunatambua michango iliyofanywa na inayofanywa na wanawake katika bara hili shukrani kubwa kwa marehemu Bibi TITI MOHAMED, Mama MARIA NYERERE, Mama GRACE MACHEL, Mama WINNIE MADIKIZZELA MANDELA , Mama SALMA KIKWETE, HELLEN SELIF JOHNSON, DKT. ASHA ROSE MIGIRO, PROF ANNA TIBAIJUKA  na wengine wote kwa michango yao iliyotupelekea tupate uhuru na maendeleo ya bara la afrika. Wanawake wote hawapaswi kukata tamaa, wanapaswa kuongeza juhudi na kuunganisha maarifa yao kwa pamoja wataleta maendeleo endelevu na kulifanya bara la afrika kwenda mbele.
Wito wetu kwenu ni kuwaasa mtumie nafasi  mnazo zipata kudumisha umoja wenu pamoja na ule wa Afrika, tusisubiri maadhimisho ya kila mwaka bali tushirikiane pamoja kila wakati na kupambana na wale wote wasio watakia mema. Ni vyema kupambana nao kwa sheria ili iweze kuwa fundisho kwa wale wanao wanyanyasa wanawake na kuwanyima haki zao za msingi. Kuliko kuwaacha na kuzidi kuwafanyia wanawake matendo maovu yasio stahili katika jamii na kuzidi kuwarudisha nyuma.
Vilevile kwa upande wa serikali za Afrika zitazame kwa umakini sekta ya afya hususani kwa upande wa   wodi za wazazi. Hospitali nyingi hazina vifaa vya kutosha ukiangalia kitanda kimoja utakuta watu zaidi ya mmoja hii ina hatarisha afya ya mama na mtoto hebu tuwe na chembe ya huruma kwa hawa mama zetu, bila ya wao tusinge kuwa hapa tulipo na jamii yeyote bila ya mwanamke haiwezi kuendelea.
Serikali ina wajibu wa  kutunga sheria itakayo mlinda mwanamke na kumpa utambulisho katika jamii kutokana mila potofu zimekuwa zikimnyima haki za kimsingi kama vile kuzuiliwa kwenda shule, kutokuwa na maamuzi katika jamii. Hivyo basi ili kumsaidia mwanamke  kuondokana na manyanyaso anayoyapata kila siku hakuna asiyejua kama mwanamke anaweza kufanya mabadiliko yaletayo tija na manufaa kwa jamii zetu tumeweza kuona baadhi yao na tuna mifano ya kuwazungumzia na kujivunia uwepo wao.
Kuna umuhimu mkubwa wa kutungwa kwa sera ya kumlinda na kumtetea mwanamke. Ni jukumu la serikali na wadau kwa kushirikiana kwa pamoja. Hii itamuwezesha mwanamke kutoka kifungoni alipo kwa muda mrefu sasa bila ya hatia yeyote, hivi ni kosa kwa wao kuwepo duniani? Au wemepoteza uhalali wa kuishi? Maana tafsiri potofu za baadhi ya watu zimewafanya wanawake kuwa kama yatima waliokosa misaada ya kimaisha. AFRICAN BROTHERHOOD FOUNDATION (ABF) imeona  “ni bora kufa kuliko kuishi na hisia zilizo kufa” kwa kulikemea hili kwa nguvu moja na kutangaza rasmi uadui na wale wote wanaomtesa na kumnyanyasa mwanamke na kuzitaka jamii zote za Afrika kushirikiana katika kumkomboa mwanake kwa nguvu moja.
Mwisho, wakati wa kusimamisha haki za wanawake umefika. Afrika ni mali ya watu wote. kuheshimiana na kuvumiliana itajenga jamii ya watu wenye fikra hai zenye mashiko ndipo maendeleo yatapatikana bila ya kupiga hodi wala foleni kwa kusubiri misaada kutoka ughaibuni. Mwanamke ndiye nguzo na mustakabali wa bara la Afrika na dunia kiujumla.
One blood, One love, One Africa forever

Tuesday, February 25, 2014

AFRIKA NA JINAMIZI LA UBINAFSI.

      Ni miaka mingi sasa toka wazee wetu,wanaharakati na wanamajumui kama Mwl J.K.Nyerere, Patrice Lumumba, Kwame Nkrumah, Booker T. Washington, Marcus Garvey na William du Bois watangulie mbele za haki. Ni ukweli usiopingika kwamba kimwili hatunao tena lakini kiroho na kifikra daima wapo pamoja nasi. Hawa wote walikuwa wazalendo na wapiganiaji haki za mtu mweusi. Siku zote walitamani kuona utu wa mtu mweusi unapatikana. Wanamajumui hawa hawakua tayari kuona mtu mweusi ananyanyaswa na kuonewa. Siku zote walipigania umoja baina ya waafrika na watu weusi kiujumla na sio maendeleo yao ili wapate utukufu binafsi( self glory). Hakika wazee wetu hawa Afrika kwao ilikua ni mwanzo na mwisho (Alfa na omega). Wanaharakati hawa kwao ilikua afrika kwanza Mimi badae...

"Gharama ya kutafuta uhuru ni bora kuliko malipo ya ukandamizaji".

        Leo hii ni miaka kadhaa tangu wanamajui hawa watangulie mbele za haki. Swali la kujiuliza ni je, viongozi wa Afrika na waafrika kiujumla wanawaenzi vipi wazee hawa? Bila shaka wazee hawa hawaenziwi tena. Falsafa za wazee hawa zimetelekezwa. Waafrika kwa bahati mbaya au kwa makusudi kabisa wamepuuza falsafa na misingi ya wazee hawa. Wazee hawa wamezikwa na misingi yao ya uzalendo, umoja,mshikamano,upendo na amani baina ya waafrika.

        Ndugu zangu, wakati wazee wetu kama kina Nyerere, Lumumba, Mandela, na Nkrumah wakiamini Afrika kwanza mimi baadae, viongozi wa sasa na waafrika walio wengi wametawaliwa na mimi kwanza nchi yangu baadae na sio Afrika tena. Asilimia kubwa ya waafrika ni wabinafsi au kwa lugha nyingine waswahili wanasema "wamimi". Wengi wanajali maslai binafsi na sio maslai ya waafrika kiujumla.

"Toka siku nyingi nia ya uovu mkubwa uliopandikizwa kwetu na wakoloni wanao ondoka, na ambao tunajipandikiza wenyewe katika hali yetu ya sasa ya utengano, ilikua ni kutuacha tumegawanyika katika mataifa yasiyojiweza kiuchumi ambayo hayathubutu kupiga hatua katika maendeleo ya ukweli.............".

       Viongozi wa Afrika hawana uchungu na bara la Afrika. Uzalendo umebaki kwenye majukwaa ya kisiasa. Uzalendo kwa viongozi waafrika na waafrika kiujumla sio tena kitu cha kujivunia. Ukosefu wa uzalendo kwa waafrika kumepelekea kuongezeka kwa rushwa Afrika, njaa, vita za wenyewe kwa wenyewe, elimu duni, magonjwa na umasikini ulio kithiri. Inasikitisha sana kuona bara la pili kwa idadi kubwa ya watu, bara la pili kwa ukubwa na bara lenye utajiri mkubwa wa rasilimali duniani linaendelea kuwa tegemezi na maskini.

         Ubinafsi kwa viongozi umepelekea wasaini mikataba mibovu yenye kuwanufaisha wao wenyewe, wajilimbikishie mali na wengine kuthubutu hata kuhamishia fedha zao kwenye akaunti za siri huko ughaibuni. Wakati viongozi wakifanya haya watoto wa shule wanakaa chini (sakafuni), shule hazina vitabu vya kutosha wala maabara. Wakati vijana wafrika wanashindwa kuendelea na masomo kwa kukosa mikopo ya vyuo vikuu, viongozi wa Afrika wameendelea kuona fahari kusafiri kwenda nchi za ulaya wakijua ndio fursa pekee ya kupiga picha na kushikana mikono na maraisi na mawaziri wakuu wa nchi kubwa zinazojiita zimeendelea.

Kwa upande mwingine waafrika ambao sio viongozi lakini wanao uwezo kifedha nao wanasakamwa na jinamizi la ubinafsi. Inasikitisha kuona matajiri wa Afrika wanatumia fedha nyingi kufadhili vyama vya siasa na wanasiasa lakini wengine wakithubutu kuwaruhusu mashabiki wa mpira wa miguu waingie bure katika viwanja kisha gharama zote atalipa yeye, lakini waafrika wangapi pale Amana hospitali wanachangia kitanda? Watoto wa shule wangapi Afrika wanakaa chini kwasababu ya ukosefu wa madawati? Kwanini hizo fedha wasiwasaidie waafrika hawa? Au kwasababu waafrika hawa wa kawaida hawana uwezo wa kutoa misamaha ya kodi kwa makampuni yao? Matajiri wakubwa wa Afrika lazima muache ubinafsi, vinginevyo Afrika itaendelea kuwaita maskini.

Inasikitisha sana kuona baadhi ya waafrika wapo tayari kutoa fedha nyingi kuwatunza waimbaji na wanenguaji wa bendi za muziki bila kujiuliza mara mbilimbili ili mradi tu wanamziki hawa wawaite "pedezyee fulani". Wakati mapedezyee hawa wakifanya hivyo,kuna waafrika Somalia wanakufa kwa njaa, vijiji kule Botswana havipitiki kwa ubovu wa barabara,waafrika katika hospitali ya Muhimbili Tanzania wanakufa kwa kukosa matibabu. Je,wanasubiri waafrika hawa waite "pedezye..." Kama wafanyavyo wanamuziki ndio wapeleke vitanda kule hospitali ya Peramiho Songea? Au madawati kule shule ya msingi Katubuka Kigoma? Waafrika mnaojiita mapedezye lazima mbadilike lasivyo Afrika itaendelea kutegemea mataifa ya kibepari wakati sisi wenyewe tukiamua tunaweza kuliendeleza bara letu.

Mwisho ningependa kutoa wito kwa waafrika wote waige mfano wa Booker T Washington aliyeamua kujitolea kujenga shule takribani 500, 'railway' kule Virginia na kuanzisha miradi mbalimbali kwajili ya kumkomboa mtu mweusi kule Marekani pasipo kuingojea serikali. Hivyo waafrika wote tuchukue jukumu la kuliendeleza bara letu bila kujali tofauti zetu za kidini, kikabila,kisiasa na kitaifa na sio kuziachia serikali peke yao.

"Afrika kwanza Mimi badae...."


One blood, one love, one Africa forever...

Friday, February 7, 2014

VIONGOZI KATIKA BARA LA AFRIKA


Kwenye kumbukumbu zangu hili neno uongozi sio suala geni hata kidogo. Kwa upande mwingine kila siku katika jamii zetu huwa tunasikia watu mbalimbali wanazungumzia yanayo husiana na uongozi kwa kutaja muhusika au wahusika wa uongozi ambao ni kiongozi au viongozi. Vilevile watu wanatafsiri neno uongozi kwa maelezo tofauti tofauti ili wapate maana.

Kona ya abfafrica inatafsiri na kuelezea maana ya uongozi; Uongozi ni dhana, taaluma inayompa muhusika madaraka, mamlaka na uwezo wa kuwawezesha wale anaowaongoza kuunganisha nguvu, ustadi na kuvitumia vipaji vyao ili kufikia malengo yao kama ni kiuchumi, kijamii ama kisiasa. Katika uongozi kuna aina ya uongozi, kama vile wakurithishana ambao mara nyingi ni utawala wa kifalme unaoendeshwa kwa njia ya urithi. Aina nyingine ni uongozi wa kuchaguliwa na watu ambao hutumia fursa ya kupiga kura kupitia chaguzi mbalimbali. Uongozi wa kimabavu daima yule mwenye mmlaka anaendesha utawala ule kwa mawazo yake bila ya kushirikisha watu anao waongoza bila ya kufuata misingi ya haki. Uongozi wa kuteuliwa na mamlaka za juu mfano raisi kumteua balozi, jaji, mkuu wa majeshi.


Kona ya abfafrica leo inapenda kuelezea juu ya uongozi wa Afrika ili kuipa jamii ya watu wa Afrika fursa ya kutambua viongozi wao waliowachagua na namna wanavyoendesha nchi zao. Uongozi bora ni ule unao simamia misingi ya utu, wenye kulenga maslahi ya watu, kutetea haki za binadamu, kuleta usawa bila ya kujali dini ama kabila la mtu. Pia viongozi wanapaswa kuwa watu wenye maadili mema yenye kulenga na kufuata taratibu na mwenendo wa kiafrika, kusimamia rasilimali za watu wanaowaongoza, kutetea watu wake na kuwapigania kwa nguvu moja, na kuwaunganisha watu wake na jamii zinazo wazunguka. 
"Ni vizuri kuongoza ukiwa nyuma na kuwaweka wengine mbele, hasa mnapo sherehekea ushindi na wakati mambo mazuri yanapotokea. Na kukaa mstari wa mbele wakati kuna hatari. Kwa kufanya hivyo, watu watauheshimu uongozi wako.
Nelson Mandela."

Swali linakuja, je, viongozi wa Afrika wanafanya haya?. Historia ya bara letu la Afrika inatuonesha namna viongozi waliopita walivyo kuwa na kiu kubwa ya kulifanya bara hili liwe moja ndio maana tarehe 25 mwezi 5 mwaka 1963 sahihi za viongozi 32 walioketi pale mjini Addis Ababa katika nchi ya Ethiopia, chini ya mwenyekiti wa kwanza hayati HAILLE SELASSIE 1, kiongozi mkuu wa Ethiopia wa wakati huo lengo ni kuinganisha Afrika katika masuala ya umoja na mshikamano wa nchi za Afrika na kuweza kuwa na sauti moja ya bara la afrika. Vilevile kuinua hali ya kimaisha ya waafrika waliotoka ndani mikono ya wakoloni, Vilevile walitaka kusaidia nchi zote zilizo kuwa bado hazijapata uhuru kuhakikisha zinakuwa huru. Mfano wa nchi hizi ni ZIMBABWE,AFRIKA YA KUSINI, ANGOLA nk. Ukitazama kwa undani viongozi wale kikubwa walichokitaka ni kufanya muungano wa kihistoria utakao lenga kupata Afrika moja.
"Mpaka itikadi inayolifanya tabaka fulani kuwa juu na jingine kuwa chini kuondolewa na kutokomezwa, kila sehemu  itakua ni vita na mpaka pale ambapo hakutakua na raia wa daraja la kwanza na wale wa daraja la plili katika taifa lolote, mpaka rangi ya ngozi ya mtu haitakuwa na tija kuliko rangi ya macho yao. Na mpaka haki za binadamu zitakapo zingatiwa kwa wote bila kujali rangi, vita itakuwepo. Na mpaka ile siku ambayo, ndoto ya amani ya kudumu, uraia wa dunia, uongozi wa maadili ya kimataifa, itabakia kuwa ndoto ya kusadika inayohitajika kutimizwa na kamwe haijafikiwa, sasa kila sehemu ni vita" Haile Selasie 1

Hata hivyo kona ya Abfafrica imebaini kuwa viongozi waliopita walifanya jitihada zao za dhati kwa ajili ya watu wao wa Afrika. Ukiangalia namna walivyo pambana na wakoloni nakuweza kuwatoa vilevile kwa kutuonesha njia ya muungano wa bara la Afrika. Leo hii viongozi walio wengi kati ya hawa tulionao wanashindwa kutimiza na kutekeleza majukumu yao kutokana wamekuwa vibaraka wa nchi za magharibi. Hii ni aibu kubwa! Hebu tazameni raia wenu wa bara hili wanavyopata tabu na kusumbuliwa huko ugaibuni! Hivi hii ndio Afrika ambayo JK Nyerere na Kwame Nkurumuah waliyo tuachia? Kumbukeni watu walijitoa sadaka kwa ajili ya bara hili. Daima tuwe tunakumbuka na kusoma historia ya nyuma. Na hivi vinavyo endelea sasa ni dhambi ya ubaguzi na unafiki tulizonazo miongoni mwetu. Tufikirieni kwa umakini wa hali ya juu kwa mitazamo chanya ili tuweze kupiga hatua. Hebu tazama hapa imefikia hatua baadhi ya vijana wa Afrika wanatamka maneno haya "Ni bora wangezaliwa mbwa Ulaya kuliko kuendelea kuishi afrika" hii sio lugha nzuri hata kidogo, ninaweza kusema ni ya kipuuzi. Lakini yote haya yanasababishwa na viongozi wetu wa Afrika kwa kushindwa kutekeleza sera zetu na kumthamini sana mtu wa nje ya bara hili. Chonde chonde viongozi wangu hebu acheni mara moja utumwa huo.

Afrika ina idadi ya watu wanakadiriwa kufika bilioni 1.033 kwa takwimu za mwaka 2013. Hebu viongozi wangu waleteni pamoja watu hawa ili tuzidi kuimarika kiuchumi. AFRICAN BROTHERHOOD FOUNDATION  ina malengo ya kukutana na viongozi wote wa Afrika ili iwakumbushe na kuweza kujitathimini tulipotoka, tulipo na tunapokwenda. Inawezekana baadhi yao ulevi wa madaraka umewalevya na kushindwa kukumbuka yale yote yalio pita. Vilevile inawataka watu wasijinasibishe kwa nchi walizo toka tu, bali ni vyema zaidi kujivunia Afrika kwasababu wote asili yetu ni moja na haiwezi katu kupotea hii ni ngao yenye upeo wa harakati zetu zilipotokea hivyo hatuna budi kujivunia na kujitukuza kabla ya kutukuzwa kwa maana hiyo afrika ni moja bila ya shaka tunapaswa kujivunia afrika yetu. 

Viongozi wote tunawaomba msiende makao makuu ya Afrika pale Ethiopia ilimradi muonekane mmeenda bali nendeni pale kwa lengo la kuutaka umoja wa Afrika una hakikisha maendeleo ya Afrika yanapatikana na maazimio yake yote yanatimizwa kwa wakati. Hii itatusaidia watu wote turudishe imani kwenu kama viongozi wetu kwasababu mtazuia wimbi kubwa la vijana lisikimbilie ugaibuni na nguvu kazi ya Afrika ikazidi kupungua. Hii italifanya bara hili kuweza kukua kiuchumi na kustawi zaidi katika ramani ya dunia.

Kuna baadhi ya viongozi wanatoka ugaibuni wanakuja Afrika kama ukiwasikiliza maneno yao, ni ya kuwakatisha tamaa waafrika wasiungane kwa sababu hilo ndio lengo lao kubwa kwa kuwa Afrika ikiungana hakuna tena gesi, mafuta, wala madini ya bure. Hivyo adui wao mkubwa ni muafrika anayejitambua na rafiki yao mkubwa ni muafrika muoga na mwenye kuzembea harakati za Afrika. 

Kona ya Abfafrica inaona ajabu sana kuona baadhi ya viongozi wa afrika wanaona wanapendwa na wale viongozi wa magharibi kumbe wanatumiwa tu kama karatasi. Napenda kuwakumbusha wako wapi akina Savimbi wa Angola na Mabutu wa Zaire? Wakishakutumia watakumaliza tu! Ombi langu kwenu tuache mara moja kuwa vibaraka, tuitazame kwanza Afrika. 

Bila ya kufanya hivyo kazi tulioachiwa na waasisi wa umoja wa Afrika, ambayo kazi kubwa ni kuhakisha Afrika inaungana na kuwa moja, maendeleo makubwa ya Afrika hayato patikana mpaka tuungane kwa ukweli. Matendo yanahitajika sana kuliko maneno. Mwendo mzima wa Afrika unapaswa uendeshwe na waafrika wenyewe. Tunamshukuru Mungu kwa kutujaalia rasilimali za kutosha vilevile kuweza kutupatia wataalamu wa fani mbalimbali hivyo basi ni jukumu kubwa la viongozi na uongozi wote wa Afrika kwa ujumla wake kuwatumia na kuwaleta pamoja watu wake. 


Mungu ibariki Afrika. One Blood, One Love, One Africa, Forever!.





Wednesday, January 29, 2014

SUDANI YA KUSINI: Machar asema tuhuma za mipango ya mapinduzi hazina "mashiko".

Ramani ya vita Sudani ya Kusini.

Kiongozi wa waasi Sudani ya Kusini ameiambia BBC tuhuma za mapinduzi juu yake na baadhi ya washirika wake hazina mashiko.

Bwana Machar ambaye kwa sasa yupo katika harakati za kukimbia amesema anategemea wajumbe katika mgogoro huu watahakikisha washirika wake wanne waliofungwa wanaachiwa.

Wachambuzi wanasema suala hili linatishia mkataba wa amani ulio sainiwa wiki iliyopita.

Mwezi Disemba Maofisa walitangaza  kwamba wanasiasa saba wanatuhumiwa kufanya jaribio la mapinduzi.

Mwanzo ulikua ni mgogoro wa kisiasa kati ya rais Salva Kiir na makamu wake wa zamani Bwana Machar tarehe 15 Disemba.

Kuanzia hapo vurugu zilianza zikapelekea vita kubwa na imeripotiwa kutokea mauaji ya kikabila.

Wanasiasa saba maarufu waliokuwa wakikiongoza chama cha SPLM walikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi mara tu baada ya madai ya kutaka kufanya mapinduzi.

katika wanasiasa hao wanne wanatuhumiwa kufanya mapinduzi na wengine saba wameachiwa katika mamlaka za Kenya ambapo walionekana wakiwa na Rais wa Kenya Uhuru Kenyata katika mkutano wa habari hapo siku ya Jumatano.

Zaidi ya watu 646,000 wamepoteza makazi toka mapigano yaanze mwezi Disemba.

Wednesday, January 22, 2014

PIGO KUBWA KWA AFRIKA BAADA YA KUMPOTEZA MWANAHABARI WETU MAHIRI, KOMLA DUMOR

Komla Dumor

Imeripotiwa; Mwanahabari wa BBC TV, Komla Dumor 41, amefariki ghafla katika nyumba yake iliyopo London.

Ni mzaliwa wa Ghana, alikuwa ni mtangazaji wa habari za BBC za dunia haswaa katika habari za Afrika.

Mtangazaji huyu alikua ni maarufu duniani, alijiunga na BBC kama mrusha matangazo ya redio mwaka 2006, baada ya kuwa mwanahabari kwa muda wa muongo mmoja huko Ghana.

Rais wa Ghana ametangaza kupitia Twitter kwamba nchi yake imepoteza moja ya "mabalozi mahiri".

Mkurugenzi wa habari za dunia BBC Peter Horrocks amemuita Komla Dumor mwongozo wa wanahabari wa Afrika  ambaye atakumbukwa sana kwa mchango wake.

"Alidhamiria kuelezea habari ya Afrika kama ilivyo" Bwana Horrocks alisema katika tamko.

"Furaha na nguvu ya Afrika huonekana kuongezeka katika kila habari aliyo eleza Komla".

"Ndugu na marafiki katika Afrika yote watakuwa na huzuni kama tulivyo sisi katika habari hii ya kuhuzunisha".

BBC imekua ikielewa kwamba Komla alikuwa akiumwa ugomjwa wa moyo.

Katika jarida la New African's magazine, la Novemba 2013, Komla alikua katika orodha ya watu 100 wenye ushawishi katika bara la Afrika. Lilisema "Komla amekuwa ni uso wa Afrika katika habari za ulimwengu na amekua na ushawishi mkubwa katika jinsi gani tunaifikia Afrika.

Komla Dumor alikua na ujuzi na mbinu za kuvutia katika utangazaji.
 James Harding, mkurugenzi wa habari na mambo ya sasa, akiongelea "jukumu pekee la Komla Dumor katika kuifikia Afrika". Alitumia uelewa, ujasiri wa hali ya juu, furaha yenye kuvutia na mvuto kwa watu katika kazi yake.

Komla Dumor alizaliwa tarehe 3 Octoba 1972 huko Accra Ghana.

Alipata bachela ya socialogy na saikolojia katika chuo kikuu cha Ghana na masta ya public administration katika chuo kikuu cha Havard.

Alipata tuzo ya mwana habari bora wa Ghana mwaka 2003 na miaka miwili baadae alijiunga na BBC.

Kuanzia hapo mpaka alikua akitangaza kipindi cha Network Afrika katika redio ya BBC world service kabla hajajiunga katika kipindi cha World Today

Komla Dumor akitangaza kipindi cha African Business Report mwaka 2009.

Mwaka 2009 Komla akawa mtangazaji wa kwanza wa kipindi cha African Business report katika habari za ulimwengu za BBC.  Pia alikua mtangazaji wa kipindi cha Focus on Africa na alifanya kazi hiyo siku moja kabla hafariki.

Alitembelea sehemu nyingi za Afrika akikutana na wajasiriamali maarufu na kuripoti mambo ya biashara yanayo endelea katika sehemu mbalimbali za baa la Afrika.

Alifanya mahojiano na wageni wa hadhi ya juu kabisa hii ni pamoja na Kofi Annan na Bill Gates.

Mwezi uliopita, alishughulika katika kutaripoti mazishi ya rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, ambaye alimwelezea kama "moja ya watu maarufu katika historia ya sasa."

Alifanya matangazo ya moja kwa moja ya matukio makubwa kama kombe la dunia la mwaka 2010 huko Afrika Kusini, mazishi ya Kim Jong-il, kuachiwa kwa mwanajeshi wa Izrael Gilad Shalit, na ndoa ya mtoto wa mfalme, William na Kate Miidleton.

Katika mjadala wa 2013 uliochapishwa mwezi jana, Dumor alisema kufariki kwa Mandela ni "moja ya vipindi vitakavyobaki na yeye".

"Kuripoti mazishi kwa mimi kumekua na kutaendelea kuwa tukio la kipekee. Taliangalia tukio hili kwa hali ya huzuni na kwa shukrani na heshima. Najiona mwenye bahati kuwa shahidi katika sehemu ile ya historia ya Mandela".

"Hajawahi kuterereka!"

Kukutana n Komla Dumor kwa mara ya kwanza mwaka 2007, mkuu wa watoa habari wa kimataifa Lyse Doucet algundua ni kwa jinsi gani mwanahabari huyo alionekana kwake.

Hajawahi kuwa muoga katika kuuliza mwaswali magumu, pia alipenda kufurahi na wengine, alisema.

Aliongeza kuwa Komla Dumor alikua na vitu vingi alivyokua napenda kama soka, imani yake na familia yake.

Ameacha mke na watoto watatu. 



Sunday, January 19, 2014

MGOGORO WA JAMHURI YA AFRICA YA KATI: MIILI YACHOMWA HADHARANI

Thomas Fessy akiripoti kutoka Bangui: Kutokuwepo kwa serikali,
sasa magenge yenye hasira yanaongoza mitaa

Genge la wakristo limewaua na kuwachoma waislam wawili huko Bangui, Jamhuri ya Afrika ya Kati. Hii ni katika mzozo wa kidini unaoendelea.

Genge hilo la majambazi limeiambia BBC kwamba litaendelea kuwaua waislam katika eneo lao.

Majeshi ya Umoja wa Afrika na Ufaransa yanajitahidi kudhibti hali ya mgogoro huo wa kiitikadi za kidini ambao ulizuka mara baada ya kundi kubwa la waasi wa kiislam kuchukua na kudhibiti nchi.

MP wanaelekea kuchagua rais wa mpito ifikapo Jumatatu wiki moja baada ya kiongozi wa waasi Michael Djotodia kuachia madaraka.

Rais huyu alitwaa madaraka baada ya kundi lake la waasi kuipindua nchi mwezi Machi mwaka jana.

Mapinduzi haya yalipelekea kuibuka kwa mgogoro wa kiitikadi za kidini kati ya wakristo wengi na waislam ambao ni wachache.

Bwana Djotodia alijiuzulu tarehe 11 January baada ya kushindwa kutuliza machafuko.

Ingawa ilionekana machafuko kama yanatulia baadaya kujiuzulu lakini imeripotiwa kutokea vurugu zaidi baada ya wiki kupita.

Ijumaa, wakala wa msaada wa afya wamesema kuwa watu wasiopungua 22 wameuliwa katika msafara wa kuwahamisha waislam kulekea Cameroon. 
Watoa msaada wa afya wakiharakisha kuiondoa miili ya waislam waliochomwa.

Genge hilo la wakristu lilimwambia Thomas Fessy wa BBC kuwa wanalipiza kifo cha mkristu mwenzao kilichotokea usiku wake. Haijulikani kama walio uawa wanahusika au wamekua walengwa kwa sababu tu ni waislam.

Baraza la Umoja wa Mataifa limethibitisha kupelekwa kwa vikosi vya Ufaransa huko CAR katika mpango wa kurejesha hali ya utulivu na hatimaye kufanyika uchaguzi kabla ya mwaka 2015.

Jumapili, bunge la mpito limetoa orodha ya wagombea nane wa urais wa mpito.

Maofisa wanasema wagombea wametimiza vigezo, mfano, hawatakiwi kuwa wanachama wa  kundi la kivita na wawe hawajawahi kufanya kazi na Djotodia wala kundi lake la waasi wa Seleka.

Katika wagombea hao yupo Meya wa Bangui na watoto wawili wa marais wa kabla, Sylivian Patasse na Desire Kolingba.