Sunday, January 19, 2014

WAKIMBIZI KATIKA BARA LA AFRIKA


Suala la wakimbizi sio suala geni kwenye vichwa vya watu wengi. Leo kama kawaida kona ya Abfafrica imeona imulike kwa kuweza kudadavua juu ya suala la wakimbizi. Kwanza kabisa kwa kutoa maana ya neno lenyewe.


 Mkimbizi ni nani?

Ni mtu au kundi la watu waliolazimika kukimbia nchi yao ili kuepuka manyanyaso, vita au vurugu. Wakimbizi huwa na hofu ya manyanyaso kutokana na rangi, dini, uraia, msimamo wa kisiasa au uanachama katika kundi fulani la kijamii. Vita na vurugu za kidini na kikabila vimekua chanzo kikuu cha wakimbizi kukimbia nchi zao.

Kuna idara maalumu iliyoanzishwa na umoja wa mataifa yenye lengo la kusimamia wakimbizi. Idara hii ni (UNHCR). Katika bara letu la Afrika nchi nyingi zenye amani zinakabiliwa na changamoto ya wakimbizi. Mfano; TANZANIA,KENYA,UGANDA,AFRIKA YA KUSINI nk. Nchi wanazotoka wakimbizi ni pamoja na Somalia, Sudan ya Kusini, Jamuhuri ya kKdemokrasia ya Kongo, Afrika ya Kati nk.  

Shirika la Umoja wa  Mataifa la Kuhudumia na Kutetea Haki za Wakimbizi

         Idara inayo shugulikia masuala ya wakimbizi (UNHCR) imeweza kutoa takwimu za idadi ya wakimbizi kwa nchi za kusini mwa jangwa la Sahara. Takwimu zinaeleza kwamba watu millioni 3.1 kwa mwaka 2012 na idadi imeongezeka kwa mwaka huu wa 2014 kwakufikia watu millioni 3.4. Watu waliopotea inakadiriwa kufikia millioni 5.4 kutoka maeneo ya nchi za Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Somalia, Sudan ya Kusini, na Mali. Vilevile watu wapatao millioni 11 wamekosa makazi. Nchini Somalia watu wanaokadiriwa millioni 2 hawana makazi na wakimbizi millioni 1 wapo maeneo ya nchi za jirani kama vile Kenya, Uganda na Tanzania. Kutoka nchini Afrika ya kati ripoti zinaonesha watu takriban 100,000 wamekimbilia nchini Cameroon  kutafuta hifadhi. 


        Mambo  yanayo sababisha wakimbizi.
  • Vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vinaweza kuwa vya kidini, kikabila na hata uasi katika jeshi. Athari zake ni kubwa sana katika jamii. Kona ya Abfafrica imebaini asilimia kubwa ya wakina mama na watoto wanapoteza maisha kutokana na suala hili. Mfano mzuri angalia nchi ya Somalia na Sudan ya Kusini, watu na jamii zao wanakumbwa na umasikini pamoja na njaa. Pia ukosefu wa elimu unatokea hali ya kuwa uchumi unazidi kuporomoka kwa kasi kubwa. 
Wananchi wakikimbia Kongo baada ya mapigano kuzidi. Oct 2008.

  • Sababu nyingine ni umasikini na njaa unapelekea watu kukimbia nchini zao. Hebu angalia nchi ya Eritrea pamoja na Ethiopia, raia wao wanakimbilia nchi nyingine. Mfano wakati wa mashindano makubwa ya kimichezo kama vile kombe la mataifa ya Afrika, kombe la Afrika mashariki na kati, baadhi ya wachezaji ambao ni raia wa nchi hizo huwa wanatoroka katika kambi za timu zao za taifa.

  • Mapinduzi ya umwagaji damu ambayo hufanywa na wanajeshi hupelekea asilimia kubwa kukimbia nchi zao. Tuliona kipindi cha Mabutu nchini Zaire na hata Liberia, Sierra Leone, Somalia na Mali. Na hapa utasikia juu ya uvunjifu wa haki za binadamu hususani watu wanapata sana mateso kama vile kubakwa na mauaji ya kimbari. 
Baada ya kutazama vitu  hivyo, kona ya Abfafrica tukiwa kama wadau na waumini wazuri wa harakati za Afrika, tunasikititishwa sana kuona Afrika kila mwaka kunatokea matukio yanayo pelekea wakimbizi. Katika suala hili la msingi kuna vitu vinaonekana kabisa kama wa Afrika tukiamua, inawezekana vikawa historia kwa kuweza kuvikomesha mara moja. Hivi ni kwanini waasi wanazidi kushika hatamu katika bara letu? Kwani hawa hatuwajui ni akina nani na wametokea wapi? Swali hili lina jibu kabisa ndani ya vichwa vya watu wote wa bara letu hili kwa kuonesha msisitizo. Hawa waasi hawatutakii heri katika bara letu ni vibaraka tu. Hebu kwa pamoja viongozi wote wakuu wa nchi zetu za Afrika, kaeni chini mtafute njia ya kuwadhibiti hawa na wapate fundisho la milele. Waasi humaliza nguvukazi ya bara hili na hutorosha rasirimali zetu. Sisi kama wapinzani wao hebu tujitolee kuwaondoa mara moja maana ndugu zetu ambao ni wakimbizi wanapata tabu. Hebu vuta taswira na kumuangalia mama yule mjamzito na mtoto mgongoni wanavyopata tabu, halafu, je, tulitafuta uhuru wa nchi za Afrika kwaajili ya waasi? Sasa wewe kama mwana wa Afrika unasababu gani ya kuunga mkono au kuwafumbia macho waasi.

Watu walio wengi wa Afrika hatuna roho za kinyama wala za kikatili ambazo daima zinabomoa mshikamano wa nafsi na imani. Hivyo basi hatuna haja sisi kama waafrika kuwanyanyasa wala kwafukuza wakimbizi wanapokimbila katika nchi zetu kutafuta hifadhi   kwasababu tukumbuke wengi wao wanakuwa wamepoteza ndugu na jamaa zao. Hivyo hatuna budi kuwapokea na kuwasaidia kwa moyo mmoja kwa kuwapa faraja itakayo wapa matumaini katika maisha yao. Tusipo wathamini hawa ndugu zetu waafrika wenzetu,  tutamkimbilia kwa nani siku matatizo yakigeukia upande wetu. Kumbukeni ardhi ya Afrika ni mali ya waafrika. Wakoloni waliligawa bara hili kwa maslahi yao wenyewe. Hivyo hatuna budi kufuata sera za kikoloni tusiwe watu wa kuiga kutoka kwa yale mabeberu yasiyo na hata chembe ya huruma kwa binadamu wenzao. 

Ombi langu kwa umoja wa Afrika (AU) wakae chini na watathimini kwa kiwango kipi wanaweza kuwaleta waafrika pamoja. Kwa sababu ukipima kwa undani mambo yanayo tokea maeneo yenye fujo na vita kwa sauti moja yanaweza kupatiwa ufumbuzi. Kikubwa hapa ni kulitazama bara la Afrika na mwenendo wake. Kipimo cha hicho ni kulileta na kulifanya bara liweze kuwa na utawala bora, uwajibikaji, usawa, haki, demokrasia ya Afrika na maadili mema kwa watu wa Afrika. Hivi ni miongoni mwa vitu ambavyo vikikosekana katika taifa fulani basi ile hali ya amani iliyokuwepo inaweza ikapotea wakati wowote. 

Kona ya abfafrica itaendelea kulisemia hili mpaka ufumbuzi wake upatikane. Vilevile tunapenda kuwashukuru wale wote wanao wasaidia hawa wakimbizi kwa kuwapa hifadhi. Sisi AFRICAN BROTHERHOOD FOUNDATION kazi yetu ni kuhakisha watu wote wa Afrika wanapata dira na mwanga katika maisha yao, na lengo kuu ni kuona Afrika inakuwa kitu kimoja na hii ndio ndoto za ndugu zetu wakimbizi pamoja na wananchi wengine wa bara hili.  Kwa ujumla wetu tukalikabili hii itatusabishia amani kurudi mara moja na kila mtu katika bara hili akajiona yupo sehemu ya salama na sauti moja ya waafrika itarudi, hii ndio kiu kubwa inayo tuandama katika jangwa hili ambalo amani yake imekuwa ikitoweka siku hadi siku. 

Waafrika sisi wenyewe tunaweza bila ya kuwezeshwa na wahisani kutoka nje. Inatupasa wenzetu wakimbizi wanavyo pata tabu na sisi tuguswe kwa namna moja ama nyingene na kwa mtazamo huu tutaweza kusaidiana kwa hatua zote tutakazo fikia. Kama ilivyo desturi yetu Afrika itajengwa na muafrika mwenyewe na kama kuibomoa tutaibomoa wenyewe. 

Narudi tena kwa hawa waasi. Hivi leo hawa jamaa wanafikiria watamuongoza nani kama wanazidi kuwaua watu wasio na hatia. Kikubwa, hawa inawezekana kabisa kuna baadhi ya serekarli zinawapa ufadhili kwasababu wana nguvu kubwa ya silaha, wamezitoa wapi? Na kwanini wanakimbilia kwenye rasirimali? Hawa wapo chini ya udhamini wa watu wasio tutakia maendeleo leo. Kwa kauli moja tunasema tena hawa ni vibaraka wa maadui wa bara la Afrika na watu wake! Shime shime viongozi wa Afrika hebu tuoneshe uzalendo kwa bara hili. Mungu ibariki Afrika!
One blood, One love, One Africa, Forever.












No comments:

Post a Comment